Msanii wa vichekesho na Muziki wa kizazi kipya nchini
Hussein Ramadhani Mkiete, almaarufu Sharo Millionea, ambaye alifariki jana
usiku majira ya saa mbili anatarajiwa kuzikwa kwao Mkoani Tanga mara baada ya
taratibu za mazishi kukamilika.
Ajali hiyo mbaya ilitokea eneo la Maguzoni Tanga baada ya
gari alilokuwa akiendesha T478 BVR
Toyota Harrier akitokea Dar es salaam kwenda Muheza kuacha njia na kupinduka
na alifariki dunia hapohapo ambapo polisi walimtambua baada ya kuona vitambulisho
vyake pamoja na picha moja ya paspot size aliyokuwanayo mfuko ambapo vitu hivyo
vyote viko polisi.
Rafiki wa karibu wa Sharo Diwani Makame Seif, akieleza
kwenye kituo kimoja cha radio alisema sharo Millionea ameumia vibaya sana
kichwani, kifuani na kwenye mikono. Pia Mjomba wa marehemu amethibitisha kuwa
Sharo Millionea atazikwa Tanga na asubuhi ya leo ratiba ya msiba itatolewa.
Ndugu na marafiki wa Sharo wameanza kwenda hospitalini baada tu ya taarifa hizi
kuwafikia. Familia ya Sharo imeshafika Hospitali ya Teule ya Tanga.
Jana usiku majira
ya saa 3:00 Kamanda wa Polisi Tanga alisema,
“leo majira ya
saa mbili usiku kwenye barabara ya Segera Muheza mtu mmoja alietambulika kwa
jina la Hussein Ramadhani au Sharo Milionea akiwa anaendesha gari namba T478
BVR Toyota Harrier akitokea Dar es salaam kwenda Muheza alipofika eneo hilo
gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake,
mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali Teule ya wilaya ya Muheza”
Kamanda amesema
hakuna kona kali sana wala ubovu wa barabara kwenye sehemu aliyopata ajali
Sharo Milionea, katikati ya Segera na Muheza ambapo gari imehifadhiwa mahali
salama kwa sababu haitembei.